[index]
swahili - kiswahili
UMOJA WA MATAIFA OFISI YA IDARA YA HABARI TAARIFA YA ULIMWENGU JUU YA HAKI ZA
BINADAMU
UTANGULIZI
Kwa kuwa kukiri heshima ya asili na haki sawa kwa binadamu wote ndio msingi wa
uhuru, haki na amani duniani,
Kwa kuwa kutojali na kudharau haki za binadamu kumeletea vitendo vya kishenzi
ambavyo vimeharibu dhamiri ya binadamu na kwa sababu taarifa ya ulimwengu ambayo
itawafanya binadamu wafurahie uhuru wao wa kusema, kusadiki na wa kutoogopa cho
chote imekwisha kutangazwa kwamba ndio hamu kuu ya watu wote,
Kwa kuwa ni lazima, ili mtu asishurutizwe kuomba msaada kutokana na maasi ya kupinga
dhuluma na uonevu, kwamba haki za binadamu ziwe chini ya ulinzi wa sheria,
Kwa kuwa ni lazima kabisa kuendeleza uhusiano wa kirafiki kati ya mataifa,
Kwa kuwa watu wa Umoja wa Mataifa wamethibitisha tena katika Mkataba wao imani
yao katika haki za asili, heshima na thamani ya binadamu na katika usawa wa haki
kwa wanaume na wanawake, na kwa sababu wamekata shauri la kuendeleza mambo ya
starehe na hali bora za maisha ya watu kwa kuwa na uhuru zaidi,
Kwa kuwa Nchi zilizo Wanachama zimeahidi, kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa,
kukuza na kuheshimu haki za binadamu na uhuru wake wa asili,
Kwa kuwa kuzitambua haki hizi na uhuru huu ni jambo la maana sana kua kutimiza
ahadi hiyo,
Kwa hiyo basi,
BARAZA KUU linatangaza
TAARIFA HII YA ULIMWENGU JUU YA HAKI ZA BINADAMU kama ndio nguzo ya juhudi kwa
watu wa mataifa yote ambayo hatimaye kila mtu na kila jamii ya watu - kwa kushikilia
daima Taarifa hiyo - watajitahidi kufundisha jinsi ya kukuza heshima ya haki hizo
na uhuru huo. Na mataifa yote yatajitahidi kuzifanya haki hizo zifahamike miongoni
mwa Nchi zilizo Wanachama na miongoni mwa watu zinaowatawala.
Kifungu cha 1.
Watu wote wamezaliwa huru, hadhi na haki zao ni sawa. Wote
wamejaliwa akili na dhamiri, hivyo yapasa watendeane kindugu.
Kifungu cha 2.
Kila mtu anastahili kuwa na haki zote na uhuru wote ambao umeelezwa katika Taarifa
hii bila ubaguzi wo wote. Yaani bila kubaguana kwa rangi, taifa, wanaume kwa wanawake,
dini, siasa, fikara, asili ya taifa la mtu, mali, kwa kizazi au kwa hali nyingine
yo yote.
Juu ya hayo usifanye ubaguzi kwa kutegemea siasa, utawala au kwa kutegemea uhusiano
wa nchi fulani na mataifa mengine au nchi ya asili ya mtu, haidhuru nchi hiyo
iwe inayojitawala, ya udhamini, isiyojitawala au inayotawaliwa na nchi nyingine
kwa hali ya namna yo yote.
Kifungu cha 3.
Kila mtu ana haki ya kuishi, haki ya uhuru, na haki ya kulindwa nafsi yake.
Kifungu cha 4.
Mtu ye yote asifanywe mtumwa au mtwana; utumwa na biashara yake ni marufuku kwa
kila hali.
Kifungu cha 5.
Mtu ye yote asiteswe, asiadhibiwe, asidharauliwe au kutendewa kinyama au kikatili.
Kifungu cha 6.
Mbele ya sheria kila mtu ana haki ya kutambulika kama mtu.
Kufungu cha 7.
Mbele ya sheria watu wote ni sawa na wanastahili haki sawa za kulindwa. Wote wana
haki sawa ya kulindwa kutokana na ubaguzi wo wote unaoweza kuvunja Taarifa hii
na mambo yo yote yanayoweza kuleta ubaguzi kama huo.
Kifungu cha 8.
Kila mtu ana haki ya kutetewa na baraza la hukumu kwa makosa ya kuvunjiwa haki
zake za asili anazostahili kwa mujibu wa kanuni na sheria.
Kifungu cha 9.
Mtu ye yote asikamatwe, asifungiwe au kuhamishwa kutoka nchi yake bila sheria.
Kifungu cha 10
Kila mtu ana haki kamili ya kuhukumiwa vyema hadharani na baraza la hukumu lililo
huru na lisilo na upendeleo katika kutoa uamuzi wa haki zake na wajibu wake na
wa makosa yo yote yanayomhusu.
Kifungu cha 11.
Kila mtu anaeshtakiwa kwa kosa la kuvunja sheria ana haki ya kuangaliwa kama si
mkosefu mpaka imethibitishwe kwa sheria, kwa kuhukumiwa hadharani, kwamba ana
hatia.
Mtu ye yote asitiwe hatiani kwa tendo lo lote au jambo lo lote ambalo halikupinga
sheria ya taifa au ya kati ya mataifa wakati alipolitenda. Wala asipewe adhabu
kali zaidi kuliko ile iliyokuwamo katika sheria wakati alipofanya kosa.
Kifungu cha 12.
Kila mtu asiingiliwe bila sheria katika mambo yake ya faragha, ya jamaa yake,
ya nyumbani mwake au ya barua zake. Wala asivunjiwe heshima na sifa yake. Kila
mmoja ana haki ya kulindwa na sheria kutokana na pingamizi au mambo kama hayo.
Kifungu cha 13.
Kila mtu ana haki ya kwenda mahali anapotaka na kuishi katika kila nchi.
Kila mmoja ana haki ya kuhama kutoka nchi yo yote, hata nchi yake mwenyewe, na
ana haki ya kurejea katika nchi yake.
Kifungu cha 14.
Kila mtu ana haki ya kukimbilia na kustarehe katika nchi nyingine kwa ajili ya
kuepukana na udhalimu.
Haki hii haiwezi kuombwa kwa udhalimu ambao hautokani na makosa ya mambo ya siasa
au na makosa ya maazimio na kanuni za Umoja wa Mataifa.
Kifungu cha 15.
Kila mtu ana haki ya utaifa.
Mtu ye yote asinyang'anywe utaifa wake bila sheria wala asinyimwe haki ya kujibadili
taifa lake kama akitaka.
Kifungu cha 16.
Watu wazima, wanaume kwa wanawake wana haki ya kuoana na kuunda jamaa bila kizuio
cho chote kwa sababu ya rangi, taifa au dini. Wana haki sawa za ndoa wakati wa
maisha yao ya ndoa na wakati wa kutenguka ndoa.
Ndoa inaweza kufungwa tu kwa hiari na mapatano kamili kati ya hao wanaotaka kuoana.
Jamaa ni kiungo cha asili cha jamii ya watu, na inastahili kulindwa na watu pamoja
na Serikali.
Kifungu cha 17.
Kila mtu ana haki ya kuwa na mali yake binafsi au kwa kushirikiana na watu wengine.
Mtu asinyang'anywe mali yake bila sheria.
Kifungu cha 18.
Kila mtu ana haki ya uhuru wa mawazo, dhamira na dini; haki hii inahusu pia uhuru
wa kubadili dini yake au imani, na uhuru wa kubainisha hadharani au faraghani-akiwa
peke yake au na watu wengine-dini yake kwa kufundisha, kwa vitendo, kuabudu na
kwa kuadhimisha.
Kifungu cha 19.
Kila mmoja ana haki ya uhuru wa kutoa na kueleza maoni yake; haki hii inahusu
pia uhuru wa kushikilia maoni yake bila kuingiliwa kati, na uhuru wa kutafuta
na kutoa habari na maoni kwa njia yo yote bila kujali mipaka.
Kifungu cha 20.
Kila mtu anayo haki ya kushiriki katika mkutano na chama kwa hali ya amani.
Mtu ye yote asilazimishwe kuwa manachama wa chama fulani.
Kifungu cha 21.
Kila mmoja anayo haki ya kushiriki katika Serikali ya nchi yake yeye mwenyewe
binafsi au kwa njia ya mjumbe aliemchagua kwa hiari yake.
Kila mmoja anayo haki sawa ya kufanya kazi katika Serikali; matakwa hayo huonyeshwa
katika uchaguzi halisi unaofanywa muda baada ya muda ambao kila mtu hupiga kura
na ambao hufanywa kwa kura ya siri na kila mtu kwa hiari yake.
Matakwa ya watu ndiyo yatakuwa msingi wa utawala wa serikali; hali hii itajidhihirisha
kwenye chaguzi za haki kwa watu wote na ambazo zinafanyika kwa siri au namna nyingine
ambayo itahakikisha uchagazi kuwa huru.
Kifungu cha 22
Kila mtu, kama raia, anayo haki ya kutunzwa na anastahili kupata hali zinazotokana
na uchumi, starehe na utamaduni-ambazo ni za lazima kwa hali bora na maendeleo
ya nafsi yake- kwa njia ya juhudi ya taifa na ushirikiano kati ya mataifa na kwa
mujibu wa utaratibu na utajiri wa kila nchi.
Kifungu ch 23.
Kila mtu ana haki ya kufanya kazi, ya kuchagua kazi aipendayo, ya kuchagua kazi
yenye masharti mazuri na ana haki ya kulindwa asikose kazi.
Kila mtu ana haki ya kupata mshahara sawa na wengine wenye kazi ya namna moja
bila ubaguzi.
Kila mfanya kazi anayo haki ya kupata mshahara wa kufaa na unaopendeza utakao
mwezesha yeye mwenyewe pamoja na jamaa yake kuishi katika hali bora, na ahifadhiwe-ikiwa
lazima- maisha yake kwa njia nyingine.
Kila mtu anayo haki ya kuunda au kujiunga na chama cho chote cha wafanya kazi
kwa ajili ya kulinda haki zake za kazi.
Kifungu cha 24
Kila mtu ana haki ya kupumzika na kufanya kazi kwa kiasi cha saa zinazostahili.
Pia ana haki ya kupata likizo, kwa vipindi, na kupokea mshahara kama vile angekuwa
kazini.
Kifungu cha 25.
Kila mtu anayo haki ya kupata hali bora ya maisha yeye mwenyewe pamoja na jamaa
yake na kupata chakula, mavazi, nyumba, matibabu na hifadhi za lazima kwa maisha
yake. Pia ana haki ya kutunzwa wakati wa kazi, wakati wa ugonjwa, wa kutojiweza,
ujane, uzee au anapokosa ridhiki yake kwa kutoweza kujisaidia.
Akina mama na watoto wanastahili kutunzwa na kupewa msaada maalum. Watoto wote-
wawe wamezaliwa katika hali ya ndoa ama hapana- lazima watunzwe vyema.
Kifungu cha 26.
Kila mtu ana haki ya kuelimishwa. Elimu yapasa itolewe bure hasa ile ya madarasa
ya chini. Elimu ya masarasa ya chini ihudhuriwe kwa lazima. Elimu ya ufundi na
ustadi iwe wazi kwa wote. Na elimu ya juu iwe wazi kwa wote kwa kutegemea sifa
ya mtu.
Elimu itolewe kwa madhumuni ya kuendeleza barabara hali ya binadamu, na kwa shabaha
ya kukuza haki za binadamu na uhuru wake wa asili. Elimu ni wajibu ikuze hali
ya kueleana, kuvumiliana na ya urafiki kati ya mataifa na kati ya watu wa rangi
na dini mbali-mbali.Kadhalika ni wajibu iendeleze shughuli za Umoja wa Mataifa
za kudumisha amani.
Ni haki ya wazazi kuchagua aina ya elimu ya kufunzwa watoto wao.
Kifungu cha 27.
Kila mtu anayo haki ya kushiriki katika maisha ya utamaduni ya jamii yo yote,
na ana haki ya kufurahia ustadi wa kazi na kushiriki katika maendeleo ya mambo
ya sayansi na faida zinazotokana nayo.
Kila mtu ana haki ya kulindwa kwa kila hali kutokana na mambo ya sayansi aliyoandika,
aliyochora au aliyogundua.
Kifungu cha 28.
Ni haki kila mtu alindwe na taratibu au kanuni za jamii na zinazohusu mataifa
mbalimbali ambazo ndani yake uhuru na haki zilizoelezwa katika Taarifa hii zinaweza
kuhifadhiwa barabara.
Kifungu cha 29.
Kila mtu ana wajibu kwa watu wa jamii yo yote ambao kati yao tu ndio yanaweza
kupatikana maendeleo kamili ya hali bora ya maisha yake.
Katika kutumia haki na uhuru wake, kila mtu itambidi kufuata kanuni zile tu zilizowekwa
na sheria kwa ajili ya kulinda heshima inayotakiwa juu ya haki na uhuru wa watu
wengine, na kwa ajili ya kuhifadhi kanuni za haki, usalama na hali njema ya maisha
katika jamii ya kidemokrasi.
Uhuru huu na haki hizi kamwe visitumiwe kinyume cha maazimio na kanuni za Umoja
wa Mataifa.
Kifungu cha 30.
Hakuna maneno yo yote katika Taarifa hii yanayoweza kubashiriwa kwamba yanaruhusu
nchi yo yote, kikundi cha watu au mtu fulani kufanya au kushughulika na jambo
lo lote ambalo nia yake ni kuharibu uhuru haki zilizoelezwa humu.
[index]