[index]
ibs
1 Corinthiens 13

1 Hata kama nikinena lugha za watu na hata za malaika, lakini kama sina upendo mimi nimekuwa tu kama sauti ya debe tupu au kengele.
2 Tena, naweza kuwa na kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, nikafahamu siri zote na kujua kila kitu; naweza kuwa na imani yote hata nikaweza kuihamisha milima, lakini kama sina upendo mimi si kitu.

3 Nikitoa mali yangu yote na kuwapa maskini, na tena nikiutoa mwili wangu uchomwe, kama sina upendo hiyo hainifai chochote.

4 Mwenye upendo huvumilia, hufadhili; mwenye upendo hana wivu, hajidai, wala hajivuni.

5 Mwenye upendo hakosi adabu, hatafuti faida yake binafsi, wala hana wepesi wa hasira; haweki kumbukumbu ya mabaya,

6 hafurahii uovu, bali hufurahia ukweli.

7 Mwenye upendo huvumilia yote, huamini yote, na hustahimili yote.

8 Upendo hauna kikomo kamwe. Kama kuna vipaji vya kutangaza ujumbe wa Mungu, hivyo vitatoweka siku moja; kama ni vipaji vya kusema lugha ngeni, vitakoma; kama kuna elimu, nayo itapita.

9 Maana ujuzi wetu si kamili, na kipaji chetu cha kutangaza neno la Mungu si kamili.

10 Lakini kile kilicho kikamilifu kitakapofika, vyote visivyo vikamilifu vitatoweka.

11 Nilipokuwa mtoto mchanga nilisema kitoto, nilifahamu kitoto, nilifikiri kitoto. Lakini sasa, maadam mimi ni mtu mzima, mambo ya kitoto nimeyaacha.

12 Tunachoona sasa ni kama tu sura hafifu katika kioo, lakini hapo baadaye tutaona uso kwa uso. Sasa ninajua kiasi fulani tu, lakini hapo baadaye nitajua yote kikamilifu, kama vile Mungu anavyonijua mimi.

13 Sasa yanadumu haya matatu: imani, tumaini na upendo; lakini lililo kuu kupita yote ni upendo.
[index]